BUNGE LA TANZANIA
OFISI YA MBUNGE WA JIMBO LA KIGAMBONI
Kumb na: KIG/KVK/VOL.1/4 29 Disemba 2011
Mhe. Dkt John P. Magufuli (MB)
Waziri
Wizara ya Ujenzi
Dar es Salaam
YAH: KUSUDIO LA ONGEZEKO LA VIWANGO VYA NAULI KATIKA KIVUKO CHA KIVUKONI-KIGAMBONI
Kichwa cha habari hapo juu chahusika.Wananchi wa Jimbo la Kigamboni wamepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kusudio la kuongeza nauli za abiria, magari na vyombo vingine vinavyotumia huduma ya kivuko kati ya Kigamboni na Kivukoni kuanzia tarehe 1 Januari 2012.
Kivuko hiki ni kiungo muhimu kwa wananchi wanaoishi upande wa Kigamboni ambao wengi wao ni watu wa kipato duni na hawana ajira za kudumu. Ongezeko la nauli kwa asilimia 100 ni kubwa sana na litawaathiri kiuchumi. Nimepigiwa simu nyingi na kuletewa malalamiko mengi katika siku ya leo kuhusiana na mpango huu wa kuongeza nauli. Wananchi wanataka kujua ni vigezo gani vilivyotumika kufikia nauli hizi mpya; vyombo gani vilivyopendekeza, kupitisha na kuidhinisha nauli hizi na wanataka kujua kwa nini hawakushirikishwa katika mjadala wa nauli mpya.
Pamoja na ongezeko kubwa la wakazi na magari yanayotumia huduma ya kivuko, cha kushangaza ni kwamba mapato kwa siku yamekuwa ni takribani Tsh 8 milioni kwa siku kwa muda mrefu sasa.
Ni dhahiri kumekuwa na upotevu mkubwa mikononi kwa watumishi wasio waaminifu wa kivuko. Mapato mengi yanapotea kwa njia zifuatazo:
1.Baadhi ya watumishi wa kivuko kukatisha risiti hususan za magari kwa kutumia vitabu bandia.
2.Baadhi ya watumishi kuziuza tena tiketi zilizotumika badala ya kuzichana.
3.Baadhi ya watumishi na askari wanapitisha magari na abiria baada ya kupokea malipo ya pembeni.
Vilevile mafuta ya vivuko huuzwa kwa wavuvi wadogo wadogo katika maeneo ya Feri.
Mambo haya yote yanafanyika pasipo kificho, binafsi nimeshawahi kushuhudia yote niliyosema hapo juu yakifanyika na kuyatolea ripoti kwa uongozi wa kivuko.
Ninaamini kuwa hatua zifuatazo zikichukuliwa mapato ya kivuko hiki yanaweza kufika zaidi ya Tsh 13 milioni kwa siku:
1.Kudhibiti uuzaji wa tiketi za abiria na magari.
2.Kudhibiti ununuzi, utunzaji na matumizi ya mafuta yanayotumika kwenye vivuko.
3.Kudhibiti idadi ya watu na magari yanayovuka bila kulipia huduma hii.
4.Kupunguza gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vibarua.
Kutokana na unyeti wa suala hili, nashauri zoezi hili lisitishwe ili kutoa fursa ya kujadiliana kuhusu upandishaji wa nauli na maboresho ya huduma hii kwa kushirikiana na wadau na wawakilishi wa wananchi katika Jimbo la Kigamboni.
Natumaini mapendekezo haya yatafanyiwa kazi ili kuepuka kuwabebesha mzigo wa gharama za uendeshaji wakazi wa Kigamboni wanaotumia huduma ya kivuko pale Feri.
Naambatanisha nakala ya barua yangu ya tarehe 19 Januari 2011 yenye kumbukumbu namba KIG/KVK/VOL.1/1 kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TEMESA ambayo ilitoa mapendekezo ya njia ya kuboresha huduma na vile vile kutaka ushirikishwaji wa wadau katika suala la ongezeko la nauli. Barua hii haijajibiwa hadi hivi sasa.
Natanguliza shukrani zangu za dhati.
Wako katika ujenzi wa Taifa
Mhe. Dkt Faustine Ndugulile (MB)
MBUNGE
Nakala:
1.Mhe. Mizengo Pinda (MB)-Waziri Mkuu
2.Mhe. Mecky Sadick-Mkuu wa Mkoa Dar Es Salaam
3.Waheshimiwa Madiwani wote-Jimbo la Kigamboni
4.Wenyeviti wa Serikali za Mitaa-Jimbo la Kigamboni
5.Mkurugenzi Mkuu-TEMESA
Habari hii nimeipakua kutoka kwenye wavuti ya Dkt Faustine Ndugulile