Maoni ya Dk. Faustine Ndugulile (Mbunge wa Kigamboni) kuhusu mchakato na muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba mpya
Nchi yetu inatimiza miaka tarehe 9.12.2011. Kwa hiyo mjadala wa kufanya mapitio ya katiba yetu umekuja muda muafaka kwa taifa hili. Ni muda mrefu umepita na hivyo ni jambo jema kutafakari tulipotoka kama Taifa, tulipo na tuendako.
Tumekuwa na katiba ya mwaka 1977 ambayo imekuwa ikutuongoza hadi hivi sasa, lakini kama taifa tumeamua kuanza mchakato utakaopelekea kuwepo na katiba mpya itakayodumu vizazi na vizazi vijavyo.
Nashukuru kuwa sehemu ya mchakato wa kupitia muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba ambayo itaongoza mchakato mzima wa kupata katiba mpya.
Kwa babati mbaya sana muswada huu umezua mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge. Baadhi ya wananchi, wanaharakati na wanasiasa wanataka muswada huu usijadiliwe kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupinga uwasilishwaji kwa mara ya pili, wananchi kutopata fursa ya kuchangia na mamlaka ya Rais kwenye mchakato huu.
Ninaungana na watanzania wote wanaotaka katiba mpya. Ninaungana na watanzania wote wanaotaka katiba nzuri na yenye kuweka maslahi yaTaifa mbele na yenye kulinda haki za msingi za Raia wa nchi.
Sasa hizi tofauti zinatoka wapi? Kwanini kumekuwa na mtazamo tofauti katika suala hili?
Jioni ya leo nimejaribu kuwasiliana na watu mbali mbali kupata mawazo na maoni yao kuhusu muswada huu unaoendelea kwa sasa. Nimegundua yafuatayo:
- Baadhi ya watu hawana ufahamu mzuri wa kitu gani kinachoendelea kwa sasa. Baadhi ya watu wanafikiri kuwa ndio tumeshaanza kuandika hiyo katiba mpya pasipo kuwashirikisha wananchi.
- Uelewa wa nini kilicho ndani ya muswada bado ni mdogo hata kwa wale wasomi.
Kimsingi kinachofanyika sasa hivi ni kutengeneza sheria itakayoweka utaratibu wa kuandaa katiba mpya. Binafsi nimeisoma mara kadhaa na ninaona inakidhi mahitaji iliyokusidiwa. Nasema hivyo kwa sababu zifuatazo:
- Maboresho yanayozingatia hoja zilizotolewa na wadau wengi zimeongezwa kwenye muswada huu.
- Nchi ya Zanzibar ambayo ni wadau wa Muungano wamepata uwakilishi wa kutosha. Raisi wa Tanzania Bara na Raisi wa Zanzibar watashirikiana katika kila hatua ya mchakato wa katiba hii. Hakuna atakayefanya maamuzi ya peke yake.
- Madaraka ya Rais yanayolalamikiwa yamepunguzwa sana kwenye muswada huu. Kwanza, Maraisi wote watashirikiana kutoa maamuzi. Pili, hadidu za rejea zimeshainishwa badala ya Raisi kuja na za kwake. Tatu, sifa na vigezo vya wajumbe wa tume zimeshainishwa.Kwa hiyo majukumu ya Raisi ni machache sana na maamuzi mengi yatafanywa na wananchi.
- Ushirikishwaji wa wananchi utakuwa ni mkubwa. Nchi nyingine zimeweza kutengeneza katiba kwa kupitia Bunge la Katiba au chakato wa kura za maoni (Referendum). Sisi Tanzania tumeamua kutumia njia zote mbili. Wananchi watashirikishwa kwa kutoa maoni yao kwenye mikutano ya tume inayosimamia mchakato wa katiba mpya, wananchi watashirikishwa kwenye mabaraza ya mapitio ya katiba, wananchi watashirikishwa kwenye Bunge la Katiba, wananchi watashirikishwa kwenye kura za maoni (Referendum).
- Muundo wa Serikali-Tungependa Serikali iwe kubwa kiasi na ya aina gani, masuala ya Serikali ya Mseto (ikiwa chama kinaongoza uchaguzi kikashindwa kupata zaidi ya nusu ya kura zote), mamlaka na madaraka ya Raisi, uthibitishaji wa Bunge kwa viongozi n.k.
- Usimamizi na uthibiti wa Rasilmali zetu kama vile ardhi, madini, gesi na kama tutabahatika kupata mafuta.
- Mfumo wa Bunge tunalotaka
- Uwakilishi wa wananchi wasio na vyama (Zaidi ya watanzania millioni 30 si wanachama wa vyama vya siasa) na suala la wagombea binafsi
- Masuala ya uwakilishi wa jinsia na makundi maalumu kwenye sehemu za maamuzi
Mchakato wa katiba ni mrefu. Niwasihi watanzania wenzangu tujadili kuhusu katiba tunayotaka pasipo kuweka masuala ya udini, maslahi binafsi, itikadi na sehemu ya Jamhuri tunapotoka. Tufanye hivi pasipo kuweka jazba na fujo. Tukifanya hivi tutafika salama. Wanaharakati watumie fursa hii kuwaelimisha wananchi haki zao na pia kuwapa elimu ya kutosha ili waweze kuchangia kwenye mjadala huu. Wanaharakati wasitumie fursa hii kufanya fujo, kuleta vurugu na kupotosha umma.
Mimi binafsi ningependa kuona tunapata katiba yenye maslahi kwa Taifa letu na vizazi vitakavyokuja baadaye. Tuna deni hilo kwao. Hatma ya Taifa hili iko mikononi mwetu. Hekima na busara zinahitajika sana wakati huu. Tutangulize Utaifa kwanza na maslahi ya nchi hii mbele.
Mungu Ibariki Tanzania
Dk. Faustine Ndugulile-Mbunge Kigamboni
15/11/2011
Dr Faustine angependa kupata maoni yako katika suala hili ili kuweza kumjenga kihoja katika kutambua watanzania wanapenda nini katika suala hilo. Kwa mtizamo chanya au hasi.
1 comment:
Kila mtu anataka katiba mpya. Tatizo linaloonekana katika kuandaa huu mswada wa namna ya kukusanya maoni, ni kama vile ulikuwa unaingiliwa ingiliwa na watu. Lakini kwa ujumla huu wa sasa ni bora sana kuliko ule wa awali.
Wanaoleta chochoko, nao hawajakosea, kwani wana wasiwasi ya kuwa wanataka kulazimishwa kitu fulani.
Mimi naungana kupinga namna ulivyoandaliwa, lakini maudhui naona yapo sawa!
Post a Comment