Member of EVRS

Monday, 21 November 2011

Ugonjwa wa Katiba Mpya Tanzania:Unatibiwa kwa Kidonge cha Rangi Mbili

Siku chache zimepita baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kuridhia muswada wa sheria utakaongoza na kuratibu jinsi ya kukusanya maoni ya katiba mpya. Japo wabunge wa Upinzani kwa idadi kubwa waliususia kabisa kwa kile kinachodaiwa kuletwa na kusomwa huku vipengele kadhaa vya sheria vikiwa vimevunjwa.  
  
Muswada ndio umeshapita, na rais Kikwete alithibitisha pale alipokuwa akiongea na "wazee wa Darisalama" japo kuna wengine hata mimi nilikuwa nawazidi umri japo sina sifa kamili ya kuitwa Mzee, nao walikuwa humo ati kama wazee! Mhesh. Rais aliahidi kuuwekea sahihi muswada uliopitishwa na wabunge (ambao kwa karibu asilimia 80 ya michango yao walikuwa nje kabisa ya muswada wenyewe), ili uwe sheria rasmi na kuanza kutumika mara moja. 
Pia aliwaagiza wabunge wa CCM mara alipokutana nao baada ya kikao cha bunge kilichoupitisha muswada huo kuwahi majimboni kwenda kueleza ujio wa neema na kiu ya katiba mpya kwa wananchi wanaowawakilisha.  
  
Hali hii ilichafuliwa na taarifa ya kamati teule ya bunge iliyoundwa kumchunguza David Jairo (ama vijana wanavyomuita DJ) kuwasilisha taarifa yao ambayo ilikuwa inachafua maana ya maadili ya kiuongozi. Kuna mapendekezo mengi tu yalitolewa ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikijumuisha wote waliotajwa kwa makosa ikiwa ni pamoja na waziri Ngeleja akidaiwa alipewa takrima ya sh. 4M ambazo ni kinyume na matumizi ya fedha za uma. 
 
Nahisi wabunge wengi wa CCM watakuwa na wakati mgumu kwenda kuiuza rasimu ya katiba itakayokuja, na mijadala itahamia kwenye pengo la uadilifu lililo onyeshwa na baadhi ya watendaji wa serikali tawala na kuwa kigezo cha kukataa vifungu vitakavyoletwa.
Kuna viashiria ambata kwa sasa kuwa mwaka 2015 utakuwa mgumu sana kwa serikali iliyopo madarakani kukubalika, labda kama kutakuwa na kipengele cha kuchomeka serikali ya umoja wa kitaifa au yaje mabadiliko makubwa sana yatakayofanyika sasa kubadili fikra za watu wanaotaka mabadiliko ya kisiasa kwa mazuri au la, yaani, people they just want a change...   
  
Kuna taarifa zisizo rasmi kwamba katibu mkuu kiongozi anatarajiwa kustaafu mwishoni mwa mwezi ujao mwaka huu, labda itakuwa ni fursa ya kuachia ngazi bila kupoteza haki zake za muda aliolitumikia Taifa, kwa wale mtakaotaka kusema muda Taifa lililomtumikia ni nyie, na wala sio mimi. 
  
Watendaji wengine wa wizara ya nishati na madini inasemekana wameanza kujiandaa kukaa benchi, na pia mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali naye inawezekana hajui nini kitafuata hasa baada ya kumsafisha DJ na baadaye kuonekana kama taarifa yake aliiandikia kwenye kituo cha daladala bila kupitia hesabu kamili ili kubaini kasoro. Pia kuna wingu la shaka kwa sasa liko juu yake kuhusu utendaji wake wa kazi, japo anasifika kwa umakini wa kwenye hesabu za halmashauri za miji na wilaya. 
  
Tunachosubiri ni Kitendawili au bomu?!!

2 comments:

Anonymous said...

Umenikumbusha kidonge cha rangi mbili ambacho zamani kilikuwa kinatumika kutibu kila aina ya ugonjwa kuanzia vidonda vya miguu, kikohozi, mapunye, homa na hata kideli cha kuku.
CCMwajue kuwa tiba ya matatizo haya si ile waliyoizoea

malkiory matiya said...

Nani atakayemwajibisha mwenzake? wakati mwenye kuwawajibisha naye anapaswa kujiwajibisha!!