Mambo ya siasa :-((
Kusema ukweli huwa ni porojo na kuteka saikolojia ya hadhira ambayo mtu anaamua kujinadi mbele yao ili iweze kumpa rungu la kuwachunga au kuwaongoza.
Najaribu kukumbuka pale ambapo "Chama Chetu Maarufu" kilipoweka hadharani nia kubwa ya kujisafisha kwa kuondoa vishubaka vya kufichia waovu ili kionekane safi tena kama kilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa.
Kikajipa miezi mitatu kuamua hatma ya wale wevi na wenye tuhuma nzito kujitoa taratibu kwa heshima na staha, vinginevyo cha moto wangekiona.
Sina hakika hicho "Chama Chetu Maarufu" kinahesabuje siku kwenye mwezi mmoja, maana kwa kalenda yetu ... tunafikiri tumeshapiga kona mbili au zaidi za hiyo miezi mitatu.
Kila mara tunasikia wimbo wa hiki "Chama Chetu Maarufu" ya kuwa hakiwezi kuendelea kukaa na watuhumiwa, ni lazima kiwakoroge na kuwamwaga, hata jana kwenye jukwaa la kisiasa, kupitia msemaji wake kilisema hadithi ile ile, ya kuwa ni lazima kitawaondoa, na ati hao ma-bazazi, wanatumia fedha nyingi sana kuhakikisha wanakikandamiza Chama Chao na kuhakikisha kinaingia kwenye kambi rasmi ya upinzani!
Nahisi huu wimbo wa kukisafisha Chama hiki, karibu utatoa vimelea sugu vya kutokusikilizwa tena, kwani hata dawa ukiitumia tu bila mpangilio kwa muda mrefu na mara kwa mara, basi vimelea huizoea na kugeuka sugu na kuendelea kuishi na kuzaana tena kwa kasi kubwa.
Tunangoja siku moja hapo hali ya kushangilia itakapobadilika na kuwa ya kuzomea, halafu sijui wasemaji nao watakuwa wameshaota usugu, na kutafsitri kuzomea huko ni kama vile kushangilia.
Basi na tuiangalie hii bendera hapo juu inavyopepea, kama ipo sawa au ni kinyume. Tuache kuangalia kama ina vitu vyote vinavyotakiwa, bali tuangalie kama kweli inasonga mbele, na imekaa sawa. Kutokea hapo, tunaweza kuamua kama tumeridhika na tunataka kuendeshwa kama bendera ilivyo au tutataka kuiweka sawa na kuendelea na kitu kilicho sahihi. Bila kusahau, tunaweza kuangalia hata na jirani yetu, ... je, naye bendera yake ipo sawa, na tunakubaliana na alivyoiweka, na je tunaweza kumuunga mkono akatuelekeza kule tunapotaka kwenda?
Tumefika wakati wa kuchagua chombo kitakachotupeleka kule tunapotaka kufika (na sio kwenda) tukiwa na imani kweli kitatufikisha, na tuachane na dhana ya kumchagua nani wa kutufikisha bila kuangalia hata uwezo wake, mabadiliko yake yenye tija, uzoefu na historia yake katika safari yetu hii ya maendeleo.
Nimeibuka tu toka usingizini nikajikuta naadika yote haya, ngoja nikapate kikombe cha kahawa nitafakari zaidi....
1 comment:
Tunahitaji mapinduzi kama haya Arab world. CCM ni chama ambacho kimepitwa na wakati.
Post a Comment