Member of EVRS

Sunday, 19 August 2012

Rada ya Utata Uwanja wa Ndege Dar es Salaam Imeharibika

Uwanja wa kimataifa wa ndege uliopo jijini Dar es Salaam kwa muda sasa umeshindwa kutoa mawasialiano ya kuongozea ndege kwa kutoa taarifa muhimu za mabadiliko ya hali ya hewa.
Habari hii niliishtukia wakati nilipokuwa naangalia matarajio ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa muda wa wiki nzima tunayoianza kupitia mtandao huu, Mtandao huu ulionyesha ya kuwa rada iliyopa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam haitoi taarifa yoyote. 
  
Rada hii hutoa vielelezo vyote muhimu vinavyohusiana na hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kiasi cha joto, hali ya unyevu, kasi na mwelekeo wa upepo, hali ya mawingu, mvua na radi. Na pia kama kutatokea mabadiliko ya ghafla, basi rada hii hutoa taarifa ili marubani wa ndege waweze kujiandaa au kutoa maamuzi ya mahali pa kutua iwapo hali ya hewa ni mbaya sana. Mbali ya yote hayo, pia rada hii hutoa taarifa ya vyombo vya anga mahali vilipo na upande vinapoelekea ili kuweza kuziongoza ndege na kufika salama sehemu zinapotarajia kutua.

Katika pitapita yangu nikakuta taarifa hii ambayo ikanihakikishia ya kuwa ni kweli rada hiyo imeharibika tangu tarehe 3 August 2012, taarifa hii ilithibitishwa na mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya hali ya hewa, ambaye alidai kuna kifaa kimeharibika ambacho kimesababisha rada hiyo kushindwa kufanya kazi. Kifaa kilichoharibika kitaweza kupatikana sehemu moja tu, kwa wale walioiuzia Tanzania rada hiyo kwa bei ya kuruka, yaani kampuni ya Uingereza (BAE Systems), ambayo ililazimika kurudisha chenji iliyojipatia kiwizi. Lakini kwa sasa, ile chenji ambayo kampuni hii ilirudisha Tanzania, itabidi itumike kwa kurudi tena kwao hao hao waliokuwa wameiibia serikali ya Tanzania ili waweze kutengeneza na kuleta kifaa kilichoharibika! 
  
Kwa sasa marubani wanategemea mawasiliano ya kizamani na kutumia akili yao binafsi hasa kwenye kutua na kuruka, kwani kasi ya upepo na ndege zilizo karibu haziwezi kuonwa na rada hii. 
  
Uwanja wa kimataifa wa ndege wa Dar es Salaam, ni mmoja wa viwanja ambavyo vina ndege nyingi zinazotua na kuruka katika ukanda huu wa Afrika mashariki, kwa hiyo kukaa bila rada kunahatarisha hali ya usalama kwa vyombo vinavyoruka katika anga la Tanzania. Wasiwasi huu umeonyeswa na matangazo ya BBC kupitia idhaa yake ya kiingereza usiku wa jumamosi 18 Agosti 2012.

No comments: