Member of EVRS

Monday, 28 May 2012

Pale Unapokutana na Mtu Usiyemtarajia!

Wiki hii nilipata mwaliko maalumu wa chakula cha usiku kutoka kwa mtu ambaye hatufahamiani.
Habari hizi nililetewa na mtu ambaye tumekwisha fanya kazi pamoja kama mara 3 hivi katika kituo cha kulelea watoto yatima na wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na wenye mtindio wa ubongo.  
  
Katika kituo hiki cha kulelea watoto yatima, nilikataa kupokea malipo yoyote kutoka kwa huyu mtu aliyeniomba nije kuwapima watoto hao na kutoa ushauri wa kitaalam. Niliamua kufanya kazi ya ujuzi wangu kwa kujitolea kutokana na mguso nilioupata baada ya kuwaona watoto wenyewe, kwani hapo awali sikudokezwa ya kuwa kuna watoto wenye ulemavu na wengine wana mtindio wa ubongo.
  
Historia niliyoipata ya mahangaiko aliyopata mtu huyu labda nimuite msamaria mwema, alijitahidi kutafuta wataalamu kwa miezi zaidi ya mitatu na walikuwa wanatoa miadi ya kuja lakini baadaye wanajitoa kwa sababu mbalimbali. Kama alivyoniambia, jiwe lake la mwisho ndio hilo alilonirushia mimi, na hakutegemea kama angepata mtu kwani alikuwa anahitaji watoto waonwe kabla ya mwisho wa mwezi huu ili kuagiza chochote kitakachowasaidia.
  
Kwangu bila kujua historia hiyo, aliponipigia simu baada ya kupata taarifa zangu kupitia ofisi za ubalozi wa Marekani hapa Kigali, nilimpa siku ya kwenda kuwaona kwani nilikuwa nina ratiba ngumu sana kwa wiki hiyo. Ilibidi nivunje ratiba yangu ya kazi kwa muda japo kwa shingo upande. Siku na saa niliyoahidi nilifika kwa muda tuliopanga hata yeye hakuwa na imani ya kwamba nitafika kutokana na uzoefu alioupata hapo awali.

Kuhusu mwaliko wa chakula cha usiku, ambao ulifanyika Jumamosi tarehe 26 May 2012 .....Nilikubali kufika kwenye hoteli ambapo nilijulishwa kuwa wameandaa meza maalum kwani ilitolewa oda maalum tangu asubuhi kwa ajili ya chakula hicho. Nilikutana na mtu huyo ambaye ni Mzungu na raia wa Marekani. Alikuja na mkewe ambaye ndio yule nilikutana naye kwenye shughuli ya kuona watoto.
Mwenyeji wangu na mkewe walionekana waungwana sana na wenye heshima. Hata walivyonipokea walionyesha kujali na kuwa waungwana, sikuwa nimezoea hali hii ya kuongozwa na kufunguliwa milango nk.  Pia, wahudumu kuwepo muda wote na kubadili hiki na kile, kama vile tupo kwenye dhifa fulani, kumbe tupo watatu tu! 
  
Tuliongea mambo mengi ya binafsi na maisha yetu hapa Rwanda. Tuligusia kidogo mambo ya uchumi na siasa. Siku ilikuwa nzuri na chakula kizuri pia.


Baadaye nilifahamishwa ya kuwa mwenyeji wangu alikuwa ni mwakilishi mkaazi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) nchini Rwanda! Na alipata habari zangu akapenda kukutana nami kwa ajili ya mazungumzo ya kawaida na kufahamiana. Japo mimi sina taaluma na mambo ya fedha wala uchumi, na shughuli zangu hazihusu masuala hayo. …… Bado ninatafakari ….. kwa nini alipenda kukutana nami, wakati shughuli zilizonikutanisha na watu wengine, taasisi yake haishughuliki moja kwa moja katika uendeshaji wake. 
  
Nimependa tu kuwasiliana nawe msomaji, ujue ya kuwa kuitika wito ni bora, japo unaweza kuichuja habari ulioitiwa au kuikataa.  

2 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

sawa kabisa bosi, yawezekana ukaulo mhajira mmoja hivi!!

harafu ngoja nikutumie inbox moja hivi

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Chib! ndo hivyo inavyokuwa hapa duniani kama sio tenda wema nenda zako basi huwa hivi. Nimefurahi sana kusoma hii na nakusifu sana kwa kuwafanyia hao watoto ulivyofanya. Mungu azidi kukubariki na uzidi kuwa na moyo huo.