Member of EVRS

Tuesday, 1 May 2012

Yaliyo Moyoni mwa JK na Mei Mosi 2012

Mei mosi 2012 ndiyo hiyo inakatika.  

  
Watu walikuwa wanatarajia kusikia neema ya mishahara kuongezwa, na ndio maana katika jiji la Tanga ambapo wafanyakazi walifanya maandamano ya mei mosi walikuwa wamejizatiti kufikisha kiu yao kwa kushika mabango yaliyokuwa na ujumbe wa “Mishahara duni, Mfumuko wa Bei na kupanda kwa gharama za Maisha” ni tatizo kubwa la wafanyakazi. 
 
Rais Kikwete ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi, hakuahidi moja kwa moja ya kuwa mshahara utapanda, bali alitoa ahadi ya kuuboresha kidogo kidogo mpaka lengo litakapofikia, japo haijulikani ni lini. 
  
Mbali ya hayo alizungumzia mjadala mkali ulioibuka mwezi uliopita bungeni juu ya taarifa za ufujaji wa fedha na raslimali za watu. Alieleza ya kuwa huo mjadala aliufurahia sana, kwani uliashiria kuwa wabunge wamekuwa makini katika kutetea mali na raslimali za Tanzania. Alisisitiza ya kuwa ni yeye ndiye aliyeamua taarifa za mkaguzi mkuu wa Serikali awe anaziweka hadharani ili kutoa fursa wabunge wazijadili kwa kina, badala ya mfumo wa zamani ambapo zilikuwa hazpewi muda wa kutosha kipitiwa na kuzijadili wakati zilikuwa na kasoro nyingi. 
  
Pia alionekana kukerwa na wizi na kutowajibika kulikofanywa nabaadhi ya watendaji wa serikali, na pia kusema ya kuwa ameipa nguvu kisheria ofisi ya mkaguzi mkuu wa Serikali kuwafikisha wahalifu wa mali za uma kwenye vyombo vya sheria pale watakapobaini matukio ya wizi hata kama ukaguzi bado unaendelea. 
  
Hakuzungumzia hatua atakazowachukulia mawaziri ambao wametajwa katika taarifa hizo, japo kuna kila dalili ya kuwa atawaondoa kama si kuwafuta kazi kwenye baraza hilo, na pia kuna uwezekano wengine wakashitakiwa kwa makosa ya jinai. 
  
Mfumo madhubuti wa kudhibiti matumizi utaanza na idara za Elimu, Afya na Maji ikiwa ni pamoja na kuweka wazi fedha zitakazokuwa zinatengwa kwa kila idara, na matumizi kutolewa taarifa kwa ngazi zote.
  
Kinachoashiria ya kuwa kuna wengine wanaweza kuwa wamekwishapoteza nyadhifa zao, ni pale mhesh. Omari Nundu alipotambulishwa zaidi ya mara mbili kama Mbunge mwenyeji wa sherehe hizo, na wala hakutajwa kama waziri huku mawaziri na manaibu waziri wengine ambao hawana kashfa walipotajwa kwa nyadhifa zao. 

No comments: