Member of EVRS

Monday 1 November 2010

Habari Mpya: Dk Ali Mohamed Shein Rais Mpya wa Zanzibar, Aahidi Seif Kuwa Makamu Wake

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imemtangaza Dr Ali Mohamed Shein wa CCM kuwa mshindi wa Urais wa Zanzibar kwa kupata jumla ya 50.1% akifuatiwa kwa karibu na Sheif Sharif Hamad wa CUF aliyepata jumla ya 49.1%, na vyama vingine viligawana 0.8%.

Seif Shariff Hamad alimpongeza Shein kwa kuchaguliwa kuwa rais mteule wa Zanzibar, na kumuomba atakapoanza kazi azingatie marekebisho katika timu ya tume ya uchaguzi, akitolea mfano kwa baadhi ya watendaji wa tume ambao walikuwa wakiharibu kwa makusudi shahada za kupiga kura hasa za watu waliokuwa wanahoji ukiukwaji wa maadili na sheria za uchaguzi zilizokuwa zinafanywa na watendaji hao. Na pia alimuomba rais mteule atambue kuwa hakuna msindi wala mshindwa, kwani ushindi ni wa Wazanzibari wote, na kumuomba rais mteule aongee na wenzake awasihi kuacha kubezana hasa baada ya utangazaji wa matokeo haya, kwani yanaweza kuleta mtafaruku.  
   
Na mwisho, alimwombea heri Rais mteule kwa Mungu ili amwongoze katika kazi zake, na kisha alikwenda kumpa mkono.   
Kusema ukweli, huu ni mfano mzuri wa kizalendo na kiungwana kwa mshindwa kukubali matokeo na kumpongeza aliyeteuliwa.   

Shein naye katika hotuba yake, baada ya kuishukuru tume na wagombea wenzake, amekiri kuwa kazi ya kuwania urais haikuwa rahisi, na ushindi wake anajua ya kuwa una changamoto za juu zinazomsubiri, na inahitaji busara kubwa katika kutekeleza uongozi mpya.  
   
Pia alijigamba kuwa hakubahatisha kugombea nafasi ya uongozi wa Zanzibar, kwani alikuwa anajiamini na alijua kuwa kazi hii angeiweza japo ni alitambua kuwa ni ngumu.  
  
Pia alimshukuru sana Maalim Saif Shariff Hamad kwa hotuba yake fupi na nzito, na amefarijika sana kutokana ana changamoto aliyoitoa Maalim, naye ameahidi kushirikiana na wazanzibari wote katika serikali mpya ya umoja wa kitaifa. Na Dk Shein, ameahidi kuisimamia serikali ya umoja wa kitaifa akishirikiana na Maalim Seif kama makamu wake.  
   
Shein ameahidi kuhakikisha kutakuwa na utulivu kama ulivyokuwa kabla ya uchaguzi, na kuwataka wazanzibari wafurahi wote kwa pamoja na kuijenga Zanzibar.

Cheo cha waziri kiongozi sasa ni kwa heri....

Mimi Nasubiri ya huku Tanganyika!!!

1 comment:

emu-three said...

Hongera sana Wazanzibar, natumai mnaingia katika hatua muhimu sana kwa maendeleo yenu na yetu pia