Member of EVRS

Monday 29 November 2010

Matumaini Mapya Wizara ya Ujenzi

Nilikuwa nikiangalia runinga leo asubuhi, nikapokea habari nzuri zinazohusu ujenzi wa barabara Tanzania. 
  
Waziri wa ujenzi, Mhesh Pombe Magufuri akiwa na naibu waziri wake Prof Harrison Mwakyembe, jana walipokuwa wakiongea na watendaji wa wizara ya Ujenzi, alitoa muda wa mwezi mmoja kwa watendaji hao kujipanga na kumletea taarifa ya matarajio (projections) ya utendaji wao wa kazi kwa kipindi kijacho. 
   
Magufuri aliyeonyesha ukali katika kauli zake, alikemea tabia ya usimamizi mbovu wa miradi ya serikali, na pia kutowajibika. 
Mbali ya yote hayo, alielekea kushangaa ni kitu gani kinachoshindikana kujenga daraja la Kigamboni, akatolea mfano wa huko Uchina ambako aliona daraja lenye urefu wa km 26 likijengwa kwa miezi 14 tu. Alitoa rai kwa NSSF kujenga daraja hilo haraka iwezekanavyo, vinginevyo ataiomba benki kuu ya Tanzania kuidhinisha na kutoa pesa za ujenzi wa daraja hilo ili serikali isimamie. Kwa hapa naona ni neema kwa wakazi na wageni wanaotembelea Kigamboni ambao wamekuwa wana kilio hiki kwa muda mrefu sasa.  
   
Cha kufurahisha zaidi, na iwapo kitakuwa cha vitendo, ni pale Magufuri aliposema uanze mpango na ujenzi wa madaraja ya juu ya kupitia magari (flyovers), kwani hakuna kinachoshindikana. Pia kuwaeleza wazi kutakuwa na ziara za kushtukiza kukagua kazi na miradi mbalimbali ya ujenzi, pale itakapokutwa kazi ya ujenzi inalegalega, basi mhandisi anayesimamia ajijue ya kuwa kibarua kimekwisha ota nyasi (Keshafutwa ajira).  
  
Na mwisho aliwagawia watendaji wote ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 - 2015 ili waweze kufahamu ni nini serikali ya CCM inakusudia kutekeleza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kutoka sasa. Na ilani hizo walizigawa yeye mwenyewe na Mwakyembe kwa mikono yao wakimpa kila mtendaji pale alipokuwa amekaa, na sio watendaji kuzifuata kwenye meza kuu.  
  
Mimi nasema, mwanzo huu unatia moyo, kwani tunawafahamu Magufuri na Mwakyembe ni watendaji wazuri na wasimamizi katika maslahi ya Taifa. Nawatakia kila la heri.

2 comments:

emu-three said...

Tatizo la barabara, Tatizo la umeme...mmh, mimi naona kama `miujiza' kama kweli litatatuliwa!
Tatizo la ardhi, miundo mbinu...mmh, sijui!
Twasubiri juhudi zenu waheshimiwa, kwani mimi nionavyo ni `kipa umbele' tu kinahitajika, na `watendaji wenye uzalendo'

José Ramón said...

Chib Thanks for visiting Creativity and imagination photos of Jose Ramon and your feedback is a very interesting blog Regards