Member of EVRS

Thursday, 2 February 2012

Egypt (Misri): Vurugu Mpirani zaua watu zaidi ya 73

Habari hii si nzuri kwa wapenzi wa soka, kwani kumetokea vurugu kubwa iliosababibisha vifo vya wapenzi wa soka 73 na wengine zaidi ya 1,000 kujeruhiwa, wengine wakiwa wamejeruhiwa vibaya. Hali hii ilitokea  katika Jiji la Port Said mara baada ya kumalizika kwa mechi ya mpira wa miguu kati ya timu zenye upinzani mkali za Al Masyr ya Port Said na Al Ahly ya Cairo siku ya tarehe 1 Februari 2012.

Mechi hii ilimalizika kwa wenyeji Al Masry kuifunga Al Ahly kwa jumla ya magoli 3-1. Tafrani ilianzishwa na mchezaji wa Al Ahly ambaye inasemekana alifanya kitendo au ishara iliyotafsiriwa kama ni ishara ya vita, hivyo kusababisha mashabiki wa timu ya Al Masyr kuingia kwenye sehemu ya kuchezea mpira (football pitch) na kuanza kuwashambulia wachezaji wa Al Ahly, ambao iliwalazimu kukimbilia kwenye vyumba vya uwanja huo. Na kwenye majukwaa ya washabiki, wale wa Al-Ahly walishambuliwa na wakalazimika kukimbilia sehemu za kutokea, hali hii ilisababisha watu kukanyagana na kuongeza idadi ya vifo na majeruhi.
  
Hakuna juhudi yoyote iliyoonyeshwa na vikosi vya usalama kwa hatua ya dharura, kiasi kwamba watu walikuwa wanashambuliana kwa kila kilichowezekana au kupatikana ikiwa ni pamoja na chupa, mawe, fimbo nk  huku wana-usalama hao wakiangalia tu.   
 
Kutokana na vurugu zilizotokea Port Said, chama cha soka cha mpira cha Misri kililazimika kufuta mechi zote ikiwa ni pamoja na mechi kati ya Zamalek na Ismailia iliyokuwa inachezwa jijini Cairo. Wakati inafutwa, ilikuwa ni wakati wa mapumziko. Kutokana na kufutwa kwa mechi hiyo, kuna wakorofi waliamua kuwasha moto kujaribu kuuchoma uwanja wa mpira huo jijini Cairo, hivyo kusababisha mkanganyiko uwanjani.  
  
Katika picha zilizokuwa zinaonyeswa na kituo cha Tv cha Misri, kilionyesha watu wakishambuliana, na wengine kujihami vichwa kwa kutumia viti ili wasipigwa na mawe kichwani! 
  
Uongozi wa Misri utakutana kwa dharura alhamisi tarehe 2 Feb  2012 kujadili kwa dharura hatua zaidi za kuchukua.  
   
Kitendo hiki ni cha aibu kwa Taifa la Misri na kinaogofya kwenye ulingo wa soka duniani.

No comments: