Member of EVRS

Wednesday 3 November 2010

Tume ya Uchaguzi Tanzania Imechoka?

Kwa mtazamo wangu, naona Tume ya uchaguzi Tanzania ndiyo inaelekea kuwa chanzo cha vurugu zote zilizotokea baada ya kupiga kura.  
  
Yote hii inatokana na kutokuwa makini kwa tume yenyewe, na kufanya kazi kwa kujiamini ya kuwa hakuna mtu yeyote atakayeweza kuwatenda kwa chochote pale watakapovuruga. Hii ni imani ya kizee, kwani ni kawaida kwetu Mzee anaposhindwa kutekeleza jambo fulani, tunamsamehe kwa misingi ya kuwa ni mzee.
  
Mapungufu yote yaliyojitokeza kwangu hayana utetezi wa msingi, suala la kusema kila siku wanajifunza halina nafasi tena, imeshatimiza zaidi ya miaka 15 tangu tume hii iundwe, na bado ati wanajifunza.   Nahisi umri wa kujifunza umeshapita kwa sasa. 
  
Walikuwa na miaka 5 ya kuandaa uchaguzi wa mwaka huu, lakini tumeshuhudia vituko na mapungufu mengi tu. 
   
  • Watu kukosekana kwenye orodha ya wapiga kura, na hivyo kunyimwa  haki yao ya kuchagua viongozi wanaowafaa
  • Kuchanganya majina na picha za wagombea
  • Kuchanganya namba za kadi za wapiga kura
  • Kuwahamisha wapiga kura kwenye vituo walivyojiandikisha bila ridhaa yao na wala bila sababu yoyote ya maana
  • Kupeleka karatasi za kupigia kura mahali pasipotakiwa
  • Kuwacheleweshea posho wasimamizi wa uchaguzi na walinzi wa vituo vya kupigia kura
  • Kuchelewesha kutoa matokeo, kwa kisingizio cha mfumo wa kurekodi matokeo, na ati miundombinu.

Ni wazi ya kuwa tume hii ina watendaji wabovu au waliochoka.
Wanapaswa kuwajibika kwa matokeo ya vurugu.
Kwa heshima yao binafsi, wanapaswa au inawabidi wapumzike sasa, kwani baadhi yao ni wazee sana kwa kazi kama hii ambayo inahitaji uangalifu mkubwa na uwezo wa kufanya kazi nyingi na kwa muda mrefu.  
  
Nina imani Filbert Bayi na Suleiman Nyambui walikuwa ni wanariadha wazuri sana wa Tanzania, lakini kwa sifa hiyo ya zamani huwezi kuwapeleka kwenye mashindano ya mbio kwa sasa, ni wazi hawatafurukuta kama utawashindanisha na wakina Kenenisa Bekele.  Labda kama unataka kupata aibu.  
  
Nina matumaini, huu ndio utakuwa mwisho wa tume hii ya Wazee wastaafu.

2 comments:

emu-three said...

Je tutajulikanaje kuwa tunafanya kazi, kama mambo yatakuwa safii, na watu wakaridhika, natumai hamtaikumbuka kabisa `tume'
Lakini sas hivi kila siku `tume' tume...tume tume...inajulikana hata na mtoto mdogo!
Mhhh, naguna kwa kutafakari!

Subi Nukta said...

Ninafurahi kuwa niliiweka habari hii kiporo na leo ndiyo nimeweza kuisoma.
Nimefurahia sana toleo hili.
Right on Chib!