Member of EVRS

Monday, 9 August 2010

Rwanda: Uchaguzi Wa Rais Waenda kwa Amani

Wananchi wa Rwanda Leo wamekuwa wanapiga kura za kumchagua rais wao kwa kipindi cha miaka saba (7) kutoka sasa.

Kiongozi wa sasa, Paul Kagame, anatarajiwa kupata ushindi wa mteremko kutokana na joto la kampeni lilivyokuwa likienda kwa takribani wiki 6 tu. Pia bado anakubalika na wananchi wengi.
Kagame alichaguliwa kwa mara ya kwanza kwenye uchaguzi wa vyama vingi miaka saba iliyopita, na alipata ushindi mkubwa sana.


Picha ya juu. Watu walipokuwa wakiingia na kutoka katika kituo cha kupigia kura leo asubuhi karibu na ninapokaa.
Upigaji wa kura unatazamiwa kusitishwa saa tisa alasiri, na shughuli za kuhesabu kura zitaanza mara moja.
Vituo nilivyotembelea kwenye muda waa saa 6 adhuhuri, nilikuta vimebakia na wapiga kura wachache, kwani inakadiriwa kwa kila kila chumba kimoja cha kupigia kura, kinatarajiwa kuwa na wapiga kura 50.
Pia kila kituo, kilikuwa kinapiga nyimbo za kuhimiza watu watumie haki yao ya kidemokrasia kupiga kura. Askari vituoni hali kadhalika walikuwa sio wengi, ukilinganisha na usiku wa kuamkia leo ambapo kulitanda askari wa jeshi la ulinzi na polisi wakipiga doria kila kona.
Jana usiku ndio ilitangazwa ya kuwa leo itakuwa ni mapumziko ili watu wapige kura, vinginevyo nasikia utaratibu wa zamani ilikuwa ni kupiga kura na kuelekea kazini.
Tunatarajia matokeo kutangazwa si zaidi ya tarehe 17 mwezi huu kadiri ya ratiba ya tume ya uchaguzi.
Uchaguzi wa wabunge ulisha fanyika, kwani wabunge huchaguliwa kila baada ya miaka 5 na Rais ni miaka 7.

5 comments:

Subi Nukta said...

Asante sana Doc Chib kwa updates. Leo asubuhi nilikusema kwenye posti yangu (http://bit.ly/b0iL25) na nikawa naomba sana Mungu utujuze yanayotokea. Asante sana.

chib said...

Ahsante Da Subi.
Yaelekea Kagame atashinda tena, maana matokeo ya awali kwenye baadhi ya vituo, amejizolea kura nyingi.

emu-three said...

Hiyo ni dalili njema, na nafikiri demokrasia ya kweli inaanza kunyemelea Africa, kwani ule uroho unaanza kufifia. Wajue kabisa wale wanaotaka madaraka kwa uroho, siku zao zitahesabika, mahakama za kimataifa zipo zitawamulika

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Vyombo vya habari vya Kimagharibi, kama kawaida, vinamshambulia Kagame vikidai kwamba haki za binadamu zimedorora nchini Rwanda tangu ashike madaraka. Vinataja kuuawa kwa Andre Rwisereka, makamu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Democratic Green Party na Jean-Leonard Rugambage, mhariri wa gazeti lililopigwa marufuku la Umuvugizi kama uthibitisho wa mkono wa chuma wa dola ya Kagame. Sijui kama madai haya yana ukweli.

Wapo pia wanaomnyoshea mkono kwamba alishiriki katika kupanga njama za kuuawa kwa Juvenal Habyarimana, hali iliyochochea yale mauaji ya halaiki.

Wote hata hivyo wanakiri kwamba pengine ndiye kiongozi makini kabisa Afrika linapokuja suala la maendeleo ya kiuchumi. Hongereni kwa kufanya uchaguzi kwa amani.

chib said...

@ Masangu. Mimi nafikiri watu hawaangalii historia ya Rwanda na kwa nini kuna kikomo cha uhuru wa vyombo vya habari.
Vyombo vya habari vilichochea sana mauaji, wale waliokuwa wapangaji wa mauaji, walitumia vyombo vya habari kueneza chuki.
Pia wananchi wengi walikubaliana na matangazo ya vyombo vya habari, na kuanza kuua. Kwenye kipindi hiki cha mpito, ikitokea tu hali fulani ya kutangaza jambo linaloleta hisia ya chuki, ni muhimu lidhibitiwe hadi watu akili zitakapopona kisaikolojia, na ndio uhuru utaongezwa.
Mbona Nyerere alitubana sana tusisikilize habari za nje, hakuna TV, hata video ilikuwa kasheshe. Aliyepinga sera zake.. ndani, lakini tulipokomaa, ndio alikuwa wa kwanza kuwatolea macho CCM kuwa wakubali vyama vingi. Mimi nafikiri ni mambo ya mpito tu. Na vyombo vya nje vinatia chumvi sana.