Member of EVRS

Friday, 11 November 2011

Dr. Hemed Abbas Kilima: Ninavyokukumbuka

Sekta ya Afya ya Tanzania imempoteza Mtaalamu aliyebobea katika fani ya macho, Dr Hemed Abbas Kilima (Pichani juu) aliyefariki jana tarehe 10 Nov 2011 kutokana na ajali mbaya ya gari.

Hayati Dr Kilima alikuwa anasafiri kutoka Mbeya kuelekea Dar es Salaam alipopata ajali hiyo pale gari aliyokuwamo ilipogongwa na basi eneo la Al-Jazeera.  
 
Ni habari ya masikitiko kwa wana-taaluma wa afya hususan upande wa macho.  
  
Dr Kilima, mpaka anapoteza uhai wake akiwa bado ni kijana wa miaka 42 tu, alishapata shahada tatu katika fani ya afya zikiwa ni pamoja na:-
  • Shahada ya udaktari wa binadamu kutoka chuo kikuu cha tiba za Afya na sayansi ya Jamii - Muhimbili
  • Shahada ya uzamili katika fani ya macho kutoka chuo kikuu cha Tumaini
  • Shahada ya afya ya jamii kwa macho kutoka London School of hygiene and tropical medicine

Mbali ya hayo, alikuwa ni
  • Daktari bingwa wa magonjwa ya macho kwa watoto (Fellow- Paediatric Ophthalmology) aliyojifunza CCBRT - Dar es Salaam.
  • Fellow wa Eastern Africa college of Ophthalmology
  • Mwenyekiti msaidizi wa chama cha madaktari na wanataaluma wa Macho Tanzania.  
  
Ninamkumbuka Dr Kilima, kwani kwenye kozi ya shahada ya uzamili kwenye fani ya macho (Master of Medicine - Ophthalmology), tulikuwa darasa moja na tulikuwa wawili tu, mimi na yeye, kwa hiyo tulipitia hatua nyingi kimasomo ikiwa ni pamoja na kusoma, kufanya kazi, kufanya tafiti na kujiandaa kwa mitihani. Mbali na hayo tulikuwa tunasafiri sehemu mbalimbali pamoja ndani na nje ya nchi katika kutekeleza majukumu ya fani yetu. 
  
Tulipeana ushauri wa mambo mengi katika masomo na kujiendeleza kitaaluma, na kama tulikuwa tunafuatana katika kisomo na kujiendeleza kama vile mmoja akibandua mguu mwenzie anafuata, na hata nilipomaliza fellowship yangu naye baadaye alijiunga na kozi kama hiyo kwa fani tofauti kidogo tu, na alihitimu vyema mwaka uliopita.  
  
Na pia ndie niliyemuachia mikoba ya Mwenyekiti msaidizi wa Chama cha madaktari na wanataaluma wa afya macho Tanzania kabla sijapata nafasi zaidi katika shirikisho la taaluma hii kwa Ukanda wa Afrika mashariki (Ophthalmological Society of Eastern Africa).  
 
Mpaka anatutoka, alikuwa ni Daktari anayefanya kazi katika hospitali ya rufaa ya Mbeya, na mratibu wa macho kwa kanda ya kusini na nyanda za juu. Hivyo, Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye bado alikuwa na muda mrefu wa kuendeleza huduma ya afya na kuwainua wengine. 
 
Binafsi nimempoteza mwenza na mshirika mkubwa kikazi, na pia nimempoteza rafiki wa karibu ambaye nilitarajia kushirikiana naye sana kuweza kuinua fani ya afya ya macho kwa Tanzania. 
  
Bwana alitoa, bwana ametwaa. 
 
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amen.

5 comments:

Subi Nukta said...

Pole sana Chibuga. Mungu akufariji.
Taaluma hii imempoteza mtu aliyehitajika katika kuokoa maisha ya wengine kutokana na maradhi yanayotibika.
Marehemu apate pumziko jema aliko.
Pole sana Pacha!

Abuu said...

R.I.P. Dr Kilima

Simon Kitururu said...

R.I.P!

Jackie said...

May the lord rest his soul in peace. We have lost a wonderful person. Still shocked by the news

malkiory matiya said...

Pole ndugu kwa kumpoteza mtu wa karibu. Mungu ailaze roho yake pema peponi.