Member of EVRS

Wednesday, 6 April 2011

Kampuni ya Simu Ya Ghaddafi Kufungwa Rasmi Rwanda

Kampuni ya mawasiliano ya simu za kiganjani ya Rwandatel inatarajiwa kusimamisha kutoa huduma za mawasiliano ifikapo usiku siku ya ijumaa tarehe 8 Aprili 2011.


Hii ni kutokana na kufutiwa leseni yake ya biashara ya mawasiliano ya simu za kiganjani hapa Rwanda baada ya kushindwa kukidhi vigezo vya biashara hiyo kwa taratibu za nchini Rwanda.
Mkuu wa tume inayodhibiti mawasiliano Rwanda (RURA) Regis Gatarayiha, amesema leseni hiyo imefungwa moja kwa moja.

Kampuni hii ya simu inamilikiwa na kiongozi mwanamapinduzi wa Libya Muhamar Ghaddafi ambaye utawala wake huko katika hatihati yakung’olewa na wapenda mabadiliko wa Libya wakisaidiwa kwa kiasi kikubwa na majeshi ya Ulaya na Marekani.

Wiki iliyopita, wakati Rais wa Rwanda Paul Kagame akiongea na waandishi wa vyombo vya habari vinavyofanya kazi Rwanda, aliulizwa msimamo wa Rwanda kuhusiana na agizo lililopitishwa na umoja wa Mataifa wa kumuwekea vikwazo vya kiuchumi Ghaddafi huku muuliza swali akilenga uwekezaji wa Ghaddafi hapa Rwanda kupitia njia ya mawasiliano. 
  
Rais Kagame alijibu kwa kueleza kuwa kampuni ya Ghaddafi tayari ilishakuwa na matatizo ya kiutendaji hata kabla ya vita ya Libya, na hivyo walikuwa wapo mbioni kuisimamisha kutoa huduma zake nchini, pia alisema anaunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa kwani nchi zote wanachama zinawajibika kufuata maagizo pale haki za binadamu zinapokiukwa.  
  
Tume inayodhibiti mawasiliano hapa Rwanda, imewashauri wateja na watumiaji wa huduma za simu wa Rwandatel kujiunga na kampuni nyingine za simu.
Wafanyakazi zaidi ya 300 watapoteza ajira zao ikijumuisha na raia wa Libya na makampuni yanayowakilisha Rwandatel nchini (Dealers).

Pia, kuna baadhi ya shule zilizokuwa zinafadhiliwa na serikali ya Libya, kwa sasa imebidi zipandishe ada kwa asilimia mia moja kukidhi upungufu wa fedha kutokana na kusimamishwa kwa malipo ya kila mwaka kutoka katika mfuko maalumu wa Libya kusaidia maendeleo ya elimu nchini Rwanda.

4 comments:

Malkiory Matiya said...

Safi sana. Rwanda ipo juu katika ketekeleza misingi ya utawala bora.

Fadhy Mtanga said...

naiunga mkono Rwanda...kwa kutekeleza azimio la UN...lakini nawasikitikia wananchi wa Rwanda kwa kuwa siasa za kimataifa zitawapa maisha magumu.

Anya said...

I hope you can use a phone from another compnay :P

hugs from us all :-)

chib said...

Hi Anya, I am using another telephone company :-)