Member of EVRS

Monday 28 June 2010

Mbinu nyingine Kwenye Ajira ya Watoto

Kumekuwa na ongezeko la ajira kwa watoto duniani.
Jitihada za kutokomeza tatizo hii inaelekea bado haijapata mafanikio makubwa.

Umuhimu wa kupiga vita ajira kwa watoto ni kwamba inawasaidia kupata muda wa kujifunza na kuweza kuwa wazalishaji mali hapo watakapokuwa wanajitegemea. Kuwakatishia fursa hii ni kuwanyima haki ya kimsingi katika maisha yao ya baadaye, na pia huchangia kuwaharibia fursa na utashi wao katika kupanga maisha yao ya baadaye.

Kwa sasa kuna aina nyingine ya ajira kwa watoto, watu wengi wameishaiona lakini labda hawajaitilia maananani au hawajatambua kwamba ni janja ya watu kuwatumia watoto katika ajira zisizo rasmi.

Jana wakati naenda na kutoka madhabahuni, nikiwa kwenye usafiri, niliona mama aliyekuwa na watoto mapacha wenye umri kama wa miezi 3 ambao walionekana kuwa na afya njema, na wakiwa wamevaa vyema. Tatizo lilikuwa ni kwamba alikuwa amewalaza pembeni ya barabara ya waenda kwa miguu chini ya kivuli kiduchu, na kwa sasa ni msimu wa kiangazi, kwa hiyo vumbi lilikuwa ni kali mno likiwatimkia hao vichanga. Toka saa 3 asubuhi nilipopita kwa mara ya kwanza na saa 6 adhuhuri nilipokuwa nikirudi walikuwa wameanikwa chini!

Sababu kubwa ya kuwaanika watoto hao hivyo ilikuwa ni kupiga mizinga (kuomba) kwa wapita njia waliokuwa wakielekea na kutoka kanisani.

Kwangu mimi naona ni sehemu ya ajira kwa watoto, kwani ni mara nyingi utakuta akina babu na bibi wakitembea mitaani na watoto wadogo na kuwashindisha njaa, na kuwaacha watoto hao wakiwa wachafu na kuchakaa kabisa kwa makusudi ili kiwe chambo cha kupewa misaada.

Ninawachukulia wanaofanya hivi kuwa ni wachoyo na wasio na huruma hata chembe. Wanapaswa kuelimishwa, na kama wanajifanya sugu, ni vizuri wachukuliwe hatua kama wale ambao huwaajiri watoto kufanya kazi.

2 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

inawezekana hata wewe ulipokuwa mdogo walifanya hivyo, kwani hujaona watoto wakizaliwa watu hupewa pesa???

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Duh!