Member of EVRS

Friday 13 July 2012

Mbunge wa Kigamboni Atolewa Bungeni kwa Kuwatetea Wananchi Wake


Mbunge wa Kigamboni Dr Faustine Ndugulile (CCM) jana tarehe 12 Julai 2012 alitolewa nje ya ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania baada ya kulazimishwa kuomba radhi na kufuta kauli ambayo aliitoa juzi kueleza wasiwasi wake wa mazingira ya baadhi ya madiwani wake kukaribishwa bungeni na waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi bila ya yeye kuwa na taarifa, na hasa ukizingatia alikuwa anajua madiwani wake walikuwa katika ziara ya mafunzo katika mkoa mwingine.

Dr Ndugulile ambaye yupo mstari wa mbele kutetea haki na stahiki za wananchi wake, amekuwa mwiba mkali kwa mawaziri ambao wamekuwa wanatumia nguvu na kuvunja sheria dhidi ya wananchi wake.
Nguvu alizonazo, zinasukumwa kwa ukubwa na matakwa ya wananchi wake ambao walimchagua kuwawakilisha katika kutatua matatizo yao mbalimbali.  
  
Mojawapo ya jambo walilomtuma kuwasemea bungeni ni pamoja na kuukataa mpango wa mji mpya wa Kigamboni kwani umegubikwa na utata mwingi na umekiuka sheria nyingi za ardhi pamoja na katiba inayotumika sasa.  
   
Wananchi hapo awali walitaka mpango huo uratibiwe upya kwa kuwashirikisha, lakini wizara husika ilikuwa inapiga chenga na kutoa taarifa ambazo hazikuwa sahihi kwenye baadhi ya vyombo vya habari na vya sheria. 
   
Inaonekana wizara na watendaji wake hawakuwa na habari ya kuwa wananchi walimwita mbunge wao katika kikao chao cha wazi na kumtuma nini akawasemee bungeni, na ndicho hicho alichokisema bungeni ambacho kinaonekana kiliwaudhi baadhi ya watendaji wa serikali na bunge na kuamua kumpa adhabu kali kwa kumkoseha siku 3 za kuhudhuria vikao halali vya bunge.  
   
Mwezi uliopita wananchi hawa hapa chini walitoa dukuduku zao na maazimio kuhusu mji wa Kigamboni

Baadhi ya wananchi wa Kigamboni walipomuita mbunge wao wamueleze dukuduku lao kuhusu mji mpya wa Kigamboni

Mwananchi akichangia mawazo kuhusu mji mpya wa Kigamboni

Mmoja wa wachangiaji aliyekuwa anawakilisha taasis ya kidini

Mwakilishi wa kamati ya wakazi wa Kigamboni akifafanua jambo kuhusu Mji Mpya unaotaka kuletwa

Viongozi wa wananchi wakisikiliza kwa makini

Mbunge akikabidhiwa ripoti ya kamati kuhusu juhudi walizozifuata na maazimio waliyoyapitisha
Katika kuonyesha kutahayari, naibu waziri wa wizara ya ardhi na maendeleo ya makazi, alionekana kwa namna fulani kuwa na kigugumizi alipokuwa akijibu baadhi ya hoja za wabunge, kwani yeye ndiye aliyekuwa mchangiaji wa kwanza baada ya Dk Ndugulile kutolewa nje ya ukumbi wa bunge.  
  
Na kudhihirisha kuwa suala hili halikumpendeza waziri, alitumia karibu theluthi moja ya muda wake wa kujibu hoja za wabunge zaidi ya 150 waliochangia kuzungumzia suala la Kigamboni na mbunge wake. Na kuonyesha ya kuwa hakupendezwa na Mbunge huyo wa Kigamboni, alikataa kumtaja Mbunge wa Kigamboni kama mmoja wa watu waliochangia katika hotuba yake aliyoitoa hapo awali. 
  
Japo waziri Tibaijuka alianza kwa kuisifia demokrasia iliyopo kwa sasa na watu kusema bila uoga, na baadaye alitamka ya kuwa amemsamehe Dr Ndugulile kwa yale aliyoyasema, lakini haikuweza kuficha kutofurahishwa na kauli ya Dr. Ndugulile na wasiwasi wake kuhusu kutekelezwa kwa mradi huo.
Sio siri, Mama Tibaijuka amekuwa mstari wa mbele kwa kutekeleza mambo kisheria, lakini kwa Kigamboni, bado hajapata ufumbuzi wa mpango huu ambao hata yeye ameukuta ukiwa tayari njiani pamoja na kasoro zake nyingi tu.  
   
Kutolewa bungeni kwa Dr Faustine kuliwashtusha wapiga kura wake, na kwa ujumla wamemuona kama shujaa wao kwa kusimama kidete kutetea maazimio yao.  
 
Kama wananchi wa nchi huru na yenye ustaarabu, hatutapenda kuona kunatokea uvunjifu wa amani kwa wana Kigamboni. Tuna imani busara na hekima itatumika kwa kufuata sheria mama za nchi.  

3 comments:

Anonymous said...

Ndio Tanzania yetu. Ukiwa mzalendo unaonekana adui wa wale wasio wazalendo.

emu-three said...

Lakini mbona hii tabia ya kutoana nje inazidi, ina maana mbunge huruhusiwi kusema yale yanayokwenda kinyume na chama chako, hata kama yanaumiza waannchi wako?

Anonymous said...

Haya ni mambo ya funika kombe mwanaharamu apete