Member of EVRS

Sunday 22 April 2012

Mnyika Apoza Machungu ya Mh. Omari Nundu

Mh. Omari Nundu

Mijadala ya Bunge letu kwa sasa sio kwamba inaudhi peke yake, bali wakati mwingine inasisimua pia.
Kama watu wengi walivyosikia taarifa ya kamati za Bunge zilizowasilishwa wiki hii, pamoja na taarifa ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali ambazo zimeainisha matumizi mabaya ya fedha za uma, pamoja na kila dalili za ufisadi hasa kwa watendaji wengi ambao huwa wanateuliwa na Rais peke yake. 
  
Taarifa hizi zilipokelewa kwa hasira kali na wabunge wote bila kujali itikadi za vyama vyao na hata kufikia maazimio ya kutaka kuleta hoja ya kutokuwa na imani na waziri mkuu iwapo mawaziri waliotajwa kuhusika na kashfa hizo hawatajiuzuru. 
 
Kikao cha Bunge cha jumamosi ya tarehe 21 Aprili 2012, kilidhihirisha mkanganyiko na ugomvi mkubwa uliomo miongoni mwa mawaziri wa serikali iliyopo madarakani, mara baada ya Waziri wa Uchukuzi, Bw. Omari Nundu kueleza bayana ndani ya Bunge ya kuwa hakuwahi kushirikishwa kwa namna yoyote na mkataba unaosemwa upo sasa wa kujenga gati namba 13 na 14 katika bandari ya Dar es Salaam. Alidai ya kwamba kisheria yeye ni mdau muhimu katika kuingia na kuidhinisha mkataba wowote unaohusiana na wizara yake. Kwa maana nyingine inaonekana waziri wa fedha alitumia mamlaka kinyume cha sheria kupitisha mkataba huo bila kumshirikisha Bwana Nundu kama ilivyotakiwa.  
Lakini kwa upande mwingine, naye waziri Nundu, alishindwa kueleza kivipi naye ana mkataba wa "mfukoni" na kampuni nyingine kutoka China, ambapo huo mkataba haujulikani na mtu yeyote isipokuwa yeye peke yake!!!!! 
  
Kikao cha jumamosi kilionekana kuwachanganya watu wote bungeni ikiwa ni pamoja na spika wa Bunge Mama Anne Makinda.

Aliyeokoa jahazi siku ya jana, labda na Taifa kwa ujumla, ni mbunge wa Ubungo, John Mnyika, ambaye alikuja na mapendekezo ya kubadili azimio la kamati inayohusiana na masuala ya uchukuzi ambayo ilitaka gati hilo lianze kujengwa mara moja, ambapo Mnyika alipendekeza upembuzi yakinifu ufanywe na taasisi inayojitegemea. Hii ilitokana na kugundulika ya kuwa mkataba uliopo kwa sasa ulifanywa na kampuni ambayo ndiyo hiyo hiyo ilikuja kupewa tenda ya kujenga gati hilo.
Hali hii ilizusha wasiwasi wa kuwepo na hali ya kuweka makadirio ya juu kupita kiasi na watu kujenga hisia au kuashiria kuwepo na dalili za rushwa ukizingatia makubaliano ya ujenzi hayakuwa na kushindanishwa, ni kama hiyo kampuni ilipewa moja kwa moja tenda ya ujenzi wa magati hayo. 
 
Kilichowafurahisha watazamaji wengi, ni jinsi Bwana Nundu alivyokuwa anashangilia kwa njia ya kibunge baada ya hoja ya Mnyika kuungwa mkono na kupitishwa ambapo ni kinyume kabisa na tulivyozoea kuona kutoka kwa mawaziri ambao mara nyingi hupinga vikali hoja za wabunge wa vyama vya upinzani!

Yaani...... kushangilia kwa mhesh. Nundu......kwangu naona hii ilikuwa ni kama ..... "haya tukose wote"

No comments: