Member of EVRS

Monday 9 January 2012

Mgogoro wa Madaktari: Umezaliwa na Kukuzwa na Wizara ya Afya na Muhimbili

Mgogoro wa madaktari unaoendelea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mimi naona ni wa kujitakia.
Madaktari walikubali kufanya kazi kwa karibu miezi miwili bila kupokea stahiki yao ya posho ya kila mwezi ambayo ni sawa na mshahara wa mtumishi yeyote, kwa maana ya kipato kwa kazi aliyoifanya mtu bila kujali ni kiasi gani.
  
Madaktari waliko mafunzoni huwa wanaitumia posho hiyo kukidhi mahitaji yao ya kimaisha kama binadamu, japo huwa ni kidogo sana kutegemea na muda wanaoutumia na mazingira wanayofanyia kazi.
Mara zote, huwa ndio wa kwanza kupokea wagonjwa muda wowote, maanake wanakuwa katika hali ya kuwa tayari kufanya kazi kwa saa 24 kila siku kwa muda wa siku 7 kwa kila wiki nk. 
  
Suala la kuwacheleweshea posho zao, ni kuwaua kisaikolojia na kumaliza nguvu zao katika kuwahudumia watu wanaohitaji huduma zao, nina maana wale ambao hawawezi kwenda mahali pengine popote kwa huduma ya kiafya, achilia mbali wale wanaoweza kwenda India nk kwa mgongo wa walipa kodi wa Tanzania. 
 
Kama Serikali ilikiri kuwa ilikuwa na ukata, kwa nini basi ilikaa kimya bila kuwataarifu madaktari hao na kuwaacha wafanye kazi bila posho kama vile wanafanya utafiti wa kisayansi kuona wataweza vipi kumudu kazi bila posho...  
 
Serikali kupitia wizara yake ya Afya na ustawi wa jamii, iliweza kupata pesa za kuwalipa posho madaktari waliopo mafunzoni na wao hawakuchelewa walirudi kazini siku hiyohiyo. 
 
Binafsi bado sijaelewa ni kwa nini Uongozi wa hospitali ya Taifa, Muhimbili uliamua kuwatimua madaktari hao 224 baada ya wao kurejea kazini kwa kuwarudisha wizara ya afya ati walikiuka mkataba wao? Huku wakifahamu kabisa watendaji wao wakuu ni hao hao madaktari waliopo mafunzoni. 
 
Kitendo hiki sijui ni cha kuwakomoa madaktari, wagonjwa au wizara iliyoshindwa kuwalipa posho!!!?
Kama wizara itaunga mkono uamuzi wa Muhimbili, basi hapo tujue kuna tatizo kubwa, kwani wizara itakuwa haijui ya kuwa taasisi yake inawakebehi na kuwadharau. Kwani ukiwa mkosaji mtu akakutupia virago vyako, maana yake hauna thamani kwake, na wala hakutaki tena, kitendo walichofanya muhimbili, ni kuitupia virago wizara ya Afya kwa kushindwa kuwalipa posho madaktari. Nitashangaa kama waziri atakenua meno na kusifia hatua ya Muhimbili huku wizara yake ikiwa imedharauliwa, labda hata na yeye mwenyewe.
   
Mimi kama mdau wa sekta ya Afya, na ndugu zangu wakiwa wanahangaika kwenye wadi wakisubiri madaktari waje wawahudumie huku wengine wakiaga dunia, na hali madaktari zaidi ya 200 ati wamezuiwa kufanya kazi, naona sio kitendo cha kiungwana kwa wananchi, na kitendo hiki hakipo katika sehemu yoyote inayohusu maadili ya taaluma ya afya duniani. Yeyote aliyefikia uamuzi huu, hastahili kuendelea kujiita mtu anayejali maslahi na afya ya wananchi wanaotegemea huduma hii. 
Ikumbukwe, gharama za kuwasafirisha madaktari hao ni kubwa, kulipia gharama zao, zitagharimu manunuzi ya dawa za wagonjwa na hivyo kuendelea kuzorotesha huduma ya afya nchini.  
   
Mwisho, naipongeza MAT kwa kuwa mstari wa mbele kujitolea kuwahudumia watu, kwani kila kukiwa na janga lolote la kitaifa linalohusu kuokoa uhai wa binadamu, MAT kupitia njia zote za mawasiliano, imekuwa ikituma ujumbe kuwaatarifu wana taaluma kukaa tayari wakati wowote kwenda kutoa msaada pale utakapohitajika, bila malipo yoyote. Na pia naipongeza kwa kutoa tamko kali kwa wizara ya Afya kuchukua hatua za haraka kulipa posho za madaktari ili wakachape kazi kuokoa maisha ya wananchi wanaotegemea huduma zao hapahapa nchini. 
  
Kuna haja ya kusafisha watu wenye dhana ya kufukuza watu tu bila kujali tatizo lilianzia wapi, na bila kupima athari zitakazojitokeza kwa maamuzi "magumu".

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Naanza kufikiria kama kweli hawa viongozi wanafanya kazi kama inavyotakiwa au ndo basi tu jina/cheo? Maana huu si uungwana kabisa.

DIGITAL WORLD PAGES ARCHIVE said...

Hello! I agree with Yasinta Ngonyani...