Member of EVRS

Thursday, 18 November 2010

CHADEMA Wamsusa Rais Kikwete na Kuondoka Bungeni

Katika hali isiyokuwa ya kutarajiwa, Wabunge wa CHADEMA leo wameondoka ndani ya ukumbi wa Bunge mara tu Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anataka kuanza kuhutubia bunge la 10. 

Kwa muda wote wakati rais anaingia na muda wa kusoma dua, wabunge wote walikuwa wametulia. Lakini mara tu rais Kikwete alipoanza kuongea, wabunge wa CHADEMA wakaamka ghafla na kutoka nje huku kukiwa na kelele za mzomeo na wabunge wa CCM wakiwaonyesha mikono kwa kupunga wakimaanisha waondoke tu! 
 
Bado sababu halisi ya kumsusa Rais Kikwete haijawekwa hadharani, japo ilikuwa inajulikana ya kuwa uongozi wa CHADEMA ulikuwa unadai rais Kikwete hakushinda kihalali kutokana na ubovu wa uendeshaji wa tume ya uchaguzi ya taifa, huku wakiwa wanaituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya uchakachuaji wa kura kutoka kwa baadhi ya maofisa wake na kuipendelea CCM huku wakiihujumu CHADEMA. 
  
Majuzi, spika wa bunge la Tanzania, Anne Makinda, aliwaita viongozi wawili wa kambi ya upinzani kutoka CHADEMA na kuwasihi wakubali kumtambua Rais Kikwete kama kiongozi halali wa Tanzania vinginevyo wanaweza kupoteza haki zao za msingi za kuwawakilisha vyema wananchi waliowachagua. Hatima ya kikao hiki cha faragha hazikujulikana wazi.

2 comments:

Fadhy Mtanga said...

kaka Chib hali hiyo ilikuwa imetarajiwa kabisa. gazeti la Tanzania Daima la leo (nimelisoma mtandaoni) lilikuwa na habari hiyo. mwenyekiti Mbowe alipoulizwa na mwandishi wa habari hiyo, aliwataka Watanzania kuwa na subira ili kuona reaction ya wabunge wa Chadema.

Sababu kubwa iliyo wazi ambayo mtu yeyote anaweza kuiona kwa macho ya kawaida, ni hali ya chama kutoyatambua matoeko ya urais kwa madai ya kuchakachuliwa kwake.

Simon Kitururu said...

Siasa bonge la lamchezo fulani vile!Tatizo tu ni kwamba ni kamchezo maumivu ya rafu wayasikiao zaidi hawako mchezoni.:-(