Member of EVRS

Sunday, 24 October 2010

Uchaguzi Tanzania 2010: Ni Heri au Kiama

Imebakia wiki moja tu kabla ya watanzania watumie haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi watakaoona wanawafaa. Ingawa sina hakika kama wengi wa wapiga kura huwa wanatafakari usemi huu.. wa kumchagua kiongozi atakayefaa, kwa maana nyingine ambaye atatimiza ndoto za jamii anayotaka kuiwakilisha.  
  
Sanduku la kura, ndio huwa linabeba siri yote ya nani kamchagua huyu, na yupi ana kura nyingi.
Kwa sisi watazamaji tunaona kijisanduku cheusi ambacho ni kama giza tu, tunasubiri kuja kutangaziwa ati kijicho bin Tamaa kashinda, na tunapiga makofi na kushangilia, yaani hatujui kwa nini tulimchagua zaidi ya kufuata upepo tu na kumeza ahadi chungu nzima bila kuangalia kama zina maslahi kwa wapiga kura.  
  
Watanzania wengi wamekuwa na hulka ya kuacha kupiga kura ati kwa kudai ni kupoteza wakati!!! Halafu wale wanaowaita ngumbaru wakipiga kura za kingumbaru na kuwashinda werevu wachache waliojitokeza kupiga kura, wale werevu ngumbaru wanakuja juu na kudai sio haki, hakushinda nk, ukiwauliza nyie mlimchagua nani, watadai kivuli (hawakupiga kura) sasa walitaka kiongozi awe hewa? Tena utakuta ambao hawakupiga kura ni wengi kuliko waliojitokeza.   Kwa nini wasiende kumuuliza huyo kivuli kwa nini hakushinda? Maana ndio chaguo lao.....   
   
Pia kuna ujinga fulani ambao watu husema .. ati ni heri ukutane na zimwi likujualo, ha ha haaa, yaani wanajua kuwa wanayemchagua kuwa ni boga tu, lakini wanaogopa kumchagua mtu mpya hata kama anaonekana yu safi kabisa. Ati wanaogopa mtafuno wake sijui utakuwaje!!  
 
Utakuta mgombea anahaidi kujenga daraja chini ya mto, na watu wanapiga makofi. Hata mgombea mwenyewe anacheka kuona haya majitu pambaf kabisa, daraja chini ya mto!!!!, yaani uchimbe chini ya mto uweke daraja, hata ukichukulia maana ya daraja haiji!  
  
Dhana ya watanzania kuogopa mabadiliko, haipo katika siasa tu, bali hata katika kufanya kazi za kimataifa, utakuta ukiwaambia njoo ujiendeleze hapa uje ujenge nchi yako baadaye kwa maarifa utakayoyapata huku, jamaa anaogopa, ati huko atapoteza kacheo kake, hata kama ni uchwara, atasingizia usalama, au hawezi kuwa mbali na mbuyu ulio jirani ya nyumba yake... yote hii ni kuogopa mabadiliko, na hivyo kila siku kukubali kuendelea kutafunwa na kazimwi kake.  
   
Ninafikiri watanzania wameweza kuwasikiliza wagombea mbalimbali wakimwaga sera zao, japo wanasiasa wajanja, wengi wamekwepa kuweka muda wa kuulizwa maswali kuhusiana na ahadi zao, ambapo nyingine ni za kufikirika tu.  
   
Mimi natoa ushauri kwa watanzania kuwa
  • Watambue kuwa kura ni siri ya mpigaji, na hakuna mtu yeyote atakayejua walimchagua nani
  • Wasiogope mabadiliko pale wanapoona yatawasaidia
  • Wawe na hulka ya kuwapima wagombea kwa yale wanayoahidi, na kama walikuwa wana nafasi hiyo kabla, wapimwe kwa yale waliyoyafanya na kama wataweza kutekeleza wanayo ahidi tena.
  • Wamchague mtu wanayefikiri ataleta maendeleo yanayoendana na eneo walilopo, sio mtu anasema atawajengea meli hapo, wakati eneo lipo kwenye sehemu ambayo hata maji ya vijito hakuna.
  • Waangalie rekodi ya uadilifu wa wagombea.
  • Watumie akili zao kutoa maamuzi na sio kuendeshwa kama punda na kubebeshwa mzigo usio na manufaa hata kidogo kwao, jaribu kufikiria punda anapobebeshwa mifuko ya sement au chumvi, unafikiri ina manufaa yoyote kwake?  
Nawatakia uchaguzi mwema hapo Jumapili ijayo. Msituangushe sisi ambao katiba yetu imetunyima uhuru wa kupiga kura.

5 comments:

malkiory said...

Asante mpiganaji kwa ujumbe huu mzito. Nakupongeza kwa hili japo upo busy na shughuli zako za kikazi hapo Marekani lakini umetufundisha kitu hapa. Ubarikiwe.

Simon Kitururu said...

Mmmmh!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

duh! utafikiri wewe utapiga kura

emu-three said...

Swadakta Chib, wewe ni mwanamapinduzi halisi , nimekubali mawazo yako, na wenye akili watayatumia

Christian Bwaya said...

Elimu murua. Nitaizingatia